KIPA namba moja wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’, amejikuta akiwa katika wakati mgumu, baada ya kupata taarifa mbaya juu ya kuvamiwa nyumbani kwake na mashabiki wanaodhaniwa kuwa ni wa Yanga.
Barthez ambaye ni kipa namba moja wa Yanga, amekuwa akituhumiwa kuwa alicheza chini ya kiwango kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Simba, baada ya timu yake kuongoza kwa mabao 3-0 lakini mechi ikamalizika kwa 3-3.
Taarifa ambazo paparazi limezipata jana asubuhi, zinasema kuwa watu hao ambao walikuwa kundi kubwa, walifika nyumbani kwa kipa huyo maeneo ya Chanika jijini Dar na kuanza kumsaka, lakini wakapewa taarifa kuwa yupo kambini.
Mara baada ya kuelezwa kuwa hayupo, watu hao ambao walionekana kuwa na hasira na kipa huyo, waliondoka eneo hilo huku majirani wakitazama kwa mbali kuona nini kitakachotokea.
Hata hivyo, baada ya Barthez ambaye ni kipa wa zamani wa Simba kujulishwa kuhusu tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia jana, aliondoka na kwenda kuihamisha familia yake na kuipeleka mafichoni baada ya kuelezwa kuwa watu hao wamepanga kurudi tena.
“Hawakuwa wastaarabu kabisa, walikuja hapa na kutaka kumfanyia vurugu, walikuja wengi, wengine wakiwa na silaha, bahati nzuri hawakumkuta.
“Unajua awali nasikia Barthez mwenyewe alishajulishwa na wasamaria wema kuwa kuna mpango wa watu kutaka kumfanyia fujo, hivyo akaihamisha familia yake,” alisema shuhuda mmoja.
Kufuatia taarifa hizo, Paparazi wetu alimtafuta Barthez, ambaye alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema anachoshukuru ni kutodhurika kwa familia yake na kusema yote anamuachia Mungu na uongozi wa klabu yake.
“Hizo taarifa ni kweli, nashukuru Mungu familia yangu ilisalimika, siwezi kuongea chochote zaidi, binafsi nasema namwachia Mungu na uongozi wa klabu kulishughulikia, ingawa limenifanya nichanganyikiwe kidogo,” alisema Barthez, aliyekuwa mnyonge mithili ya mtu aliyeua.
DEAR READER LEAVE A COMMENT BELOW
SHARE THIS POSTS TO YOUR FRIENDS BELOW==>>
DONT HESITATE TO JOIN OUR FACEBOOK PAGE BELOW FOR MORE BREAKING AND HOT RESEARCHED NEWS