Wagonjwa wakiwa wamepumzika katika mazingira duni sana ndani ya moja ya zahanati za umma zilizoko maeneo ya vijijini. Wengi wako katika hatari kubwa kwani uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha mfumo mzima wa kitabibu Tanzania umeoza, huku wagonjwa wakitumbukia katika makucha ya madaktari na wafamasia feki, wanaotoa vipimo visivyofaa, na dawa zisizokidhi viwango.Baadhi ya wauzaji wa dawa za binadamu kwenye maduka wanawauzia wateja wao dawa tofauti na zile walizoandikiwa kwenye vyeti na madaktari kwa maelezo kuwa walizonazo ni bora zaidi au ni za aina moja ila zimetengenezwa na viwanda tofauti.
Wiki iliyopita tuliona ushuhuda wa daktari feki aliyejitambulisha kwa jina la Ramla Maganga (siyo jina lake halisi), akieleza namna alivyokuwa akihudumia wagonjwa kwenye zahanati binafasi wilayani Temeke, Dar es Salaam. Inaendelea…
Madhara yatokanayo na madaktari feki
Daktari bingwa wa upasuaji, Hospitali ya Aga Khan, Dk Aidan Njau anasema madaktari feki wanasababisha madhara makubwa kwa wagonjwa kwa kuwa wanatumia uzoefu badala ya taaluma ya matibabu.
“Hawa watu wanatoa dawa kwa mazoea, baadhi yao wamefanyakazi wodini kama manesi kwa miaka 10 hadi 20 wakiwaona madaktari wanavyotoa dawa. Wengine wamefikia hata hatua ya kuwa na vibanda vya dawa mitaani,” alisema.
Anasema kwamba baadhi ya madaktari hao huwapa wagonjwa dawa chini ya kipimo kinachotakiwa, hivyo kuwafanya washindwe kupona, huku wengine wakizidisha dozi na kusababisha madhara kwenye maini na figo.
“Wanatoa dawa bila kufanya vipimo. Mgonjwa anapewa dawa ya maumivu anameza, baada ya mwezi anagundulika kuwa ana saratani. Mtu mwingine anasema anasikia maumivu tumboni anapewa dawa ya maumivu, kumbe ni Appendisitis (shambulizi la kidole tumbo) baadaye kinapasuka. Mbaya zaidi baadhi yao wanauza dawa zilizokwisha muda wake,” anasema.
Maduka ya dawa yanauza dawa tofauti
Baadhi ya wauzaji wa dawa za binadamu kwenye maduka wanawauzia wateja wao dawa tofauti na zile walizoandikiwa kwenye vyeti na madaktari kwa maelezo kuwa walizonazo ni bora zaidi au ni za aina moja ila zimetengenezwa na viwanda tofauti.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwenye maduka kadhaa ya dawa muhimu, umebaini kuwa baadhi ya wauzaji kwenye maduka hayo huwalazimisha wateja wao kununua dawa tofauti ambazo hazina uwezo wa kutibu ugonjwa husika.
Mwandishi wetu alitumia cheti cha mgonjwa aliyeandikiwa dawa aina ya Clarithromycin kuzunguka kwenye maduka mbalimbali ya dawa, lakini kila alipokwenda aliuziwa dawa zenye majina tofauti huku akiambiwa kuwa zote zinatibu ugonjwa ya aina moja.
Katika duka la kwanza lililopo Mbagala Kuu, wilayani Temeke, muuzaji ambaye hakufahamika jina lake, alipoulizwa kama ana dawa ya Clarithromycin alijibu kuwa anayo. Hata hivyo, alileta dawa aina ya Erythtromycin na kumkabidhi mwandishi bila maelezo yoyote.
Alipoulizwa mbona dawa hiyo ni tofauti na ile aliyoandika daktari, muuzaji huyo alisisitiza kuwa zote zina nguvu sawa ila zimetengenezwa na kampuni tofauti.
-MWANANCHI
DEAR READER LEAVE A COMMENT BELOW
SHARE THIS POSTS TO YOUR FRIENDS BELOW==>>
DONT HESITATE TO JOIN OUR FACEBOOK PAGE BELOW FOR MORE BREAKING AND HOT RESEARCHED NEWS