Mapigano mapya yamezuka jana Jumamosi(26.10.2013) kati ya majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na waasi katika siku ya pili ya machafuko ambayo yamesababisha miito ya utulivu kutoka kwa jumuiya ya kimataifa .
Mapigano ya hivi karibuni mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yamezuka siku ya Ijumaa, chini ya wiki moja baada ya serikali mjini Kinshasa na waasi wa kundi la M23 kutangaza kuwa mazungumzo ya amani mjini Kampala yamevunjika.
Jeshi la serikali jioni ya Jumamosi lilisema kuwa limeukamata mji wa Kibumba , mji ulioko kilometa 25 kaskazini ya eneo mji wa mashariki mwa nchi hiyo wa Goma ambao unatoa njia kuelekea katika eneo la waasi upande wa kaskazini.
"Kibumba uko chini ya udhibiti wa jeshi la serikali FARDC kuanzia leo," afisa mwandamizi wa jeshi ameliambia shirika la habari la AFP mjini Goma. Waasi hawakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia tamko hilo.
Upande mwingine wa mapigano umeanza ghasia siku ya Jumamosi wakati jeshi liliposhambulia maeneo ya kundi la M23 katika jimbo la Mabenga, kiasi ya kilometa 80 kaskazini mwa goma na karibu na mpaka na Uganda.(P.T)
Jeshi "limeanzisha mashambulizi katika barabara ya Mabenga kuelekea Kahunga. Linatumia wanajeshi, vifaru na makombora", afisa mwingine wa jeshi amesema, akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina.
Waasi wamethibitisha kuwa mapigano yamesambaa hadi katika eneo la kaskazini.
Mapigano yasambaa
"Mapigano yanaongezeka katika maeneo yote," kiongozi wa kisiasa wa M23 Bertrand Bisimwa amesema katika tovuti ya kundi hilo.
Mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika mzozo huo, Mary Robinson na Martin Kobler, wametoa taarifa wakielezea wasi wasi wao mkubwa kuhusiana na mapigano hayo mapya.
"Tunatoa wito kwa pande zote kuonyesha hali ya uvumilivu na kuanza tena majadiliano mjini Kampala," wamesema. Marekani imesema kuwa imesitushwa na ripoti za kuongezeka kwa mapigano, licha ya miito ya kimataifa kwa pande hizo kuonesha hali ya kuvumiliana.
"Tunawasi wasi mkubwa juu ya ripoti za mapigano ya mpakani, " katika jimbo la Kivu ya kaskazini, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Jen Psaki amesema katika taarifa, akizitaka pande zinazopigana, "kuacha vitendo vitakavyozidisha hali hiyo".
Taarifa ya Psaki imezitaka pande hizo kurejea katika majadiliano, " ili kuondoa vikwazo vilivyobaki kuelekea kutiwa saini kwa makubaliano ya mwisho, na ya msingi, ambayo yataleta usitishaji wa kudumu wa mapigano na kuwawajibisha wake ambao wamefanya uhalifu mkubwa".
Jumuiya ya kimataifa yaonya
Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton pia ametoa wito, "kwa wahusika wote katika eneo hilo kuzuwia kuongezeka zaidi kwa hali hiyo na kuufanya mzozo huo wa kimataifa".
Athari zilizoripotiwa ndani ya mpaka wa Rwanda kutokana na matukio ya hivi karibuni yanapaswa kufanyiwa uchunguzi kwa pamoja," amesema Ashton.
Waasi wanadai kuwa jeshi la serikali lilishambulia maeneo yao mapema siku ya Ijumaa, lakini jeshi la serikali linasisitiza kuwa lilishambuliwa kwanza, madai ambayo yanaungwa mkono na duru kutoka ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO.
Wakati huo huo jeshi la serikali ya Congo limesema limepata mafanikio makubwa dhidi ya waasi wa M23 katika siku ya pili ya mapigano makali jana Jumamosi na kuitaka nchi jirani ya Rwanda kusaidia kuwanyang'anya silaha waasi.
DEAR READER LEAVE A COMMENT BELOW
SHARE THIS POSTS TO YOUR FRIENDS BELOW==>>
DONT HESITATE TO JOIN OUR FACEBOOK PAGE BELOW FOR MORE BREAKING AND HOT RESEARCHED NEWS