Tuesday, October 22, 2013

Tanzania yawalaumu waasi wa M23 kwa kuifanya itengwe jumuiya ya Africa Mashariki


KUNDI la waasi wa M23, linalopambana na Jeshi la Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), limetajwa kuwa chanzo cha kuisambaratisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Kauli hiyo imetolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, katika mahojiano yake na kituo cha redio cha Clouds.

Membe amesema kinachosababisha Tanzania itengwe na baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya ya EAC, ni hatua yake ya kupeleka majeshi katika mji wa Goma ulio Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa ajili ya kupambana na waasi wanaoipinga Serikali ya Rais Joseph Kabila.

Amesema hatua hiyo ya Tanzania ilizikera baadhi ya nchi wanachama wa EAC, zenye maslahi ya moja kwa moja na kundi hilo na kusisitiza kuwa hata kama itatengwa, kamwe haitaondoa vikosi vyake DRC na badala yake vitaendelea kupambana.

“Najua sababu za wenzetu kuharakisha shirikisho la kisiasa na kuamua kufanya vikao vya siri vya kuitenga Tanzania, ni uamuzi wetu wa kupeleka vikosi vya kijeshi Congo, wanalalamika kwamba ni kwanini tumefanya hivyo na kudai kuwa maamuzi yetu hayo yatauvunja umoja wetu, sisi tukawaambia hatuwezi kuacha kuleta amani Kongo, hiyo ndiyo sababu,” alisema Membe.

Aliitaja sababu nyingine inayotishia uhai wa jumuiya hiyo kuwa ni uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kukataa suala la ardhi kuingizwa katika mambo ya pamoja ya jumuiya.

“Sisi ni nchi kubwa, tuna kila kitu, tuna ardhi kubwa, hatuendeshi nchi yetu kwa muungano wa makabila, wenzetu wanatuonea wivu, wanaitaka ardhi yetu, Mzee Kikwete amekataa, wanaamua kututenga, niwahakikishie Watanzania, hatuna hofu hata chembe na suala hili.

“Hawa jamaa pia wanakerwa na hatua yetu ya kuwepo kwenye Jumuiya ya SADC, wanaona kama tunafaidi sana, lakini niwaambie kwamba hatuwezi kutoka SADC, mbona wao wako COMESA,” aliongeza Membe.

Aidha Membe aligusia ujio wa viongozi wa Kimataifa nchini Tanzania kuwa moja ya sababu za nchi wanachama wa EAC kuitenga Tanzania, kwa madai kuwa inafanya mambo yake yenyewe.

Kwa miezi kadhaa kumekuwa na jitihada zinazofanywa na marais wa Rwanda, Kenya na Uganda za kutaka kuunda shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki pasipo kuishirikisha Tanzania.

Tayari marais hao wamekwishaanzisha mipango ya pamoja ya kiuchumi na kuimarisha miundombinu ya reli na bandari, ambapo mwezi Agosti mwaka huu walikutana mjini Mombasa kwa ajili ya uzinduzi wa gati namba 19 la kuingiza na kutoa mizigo katika Bandari ya Mombasa.

Taarifa nyingine za hivi karibuni kutoka nchini Rwanda zimeeleza kuwa nchi hizo tatu zimekwishaunda kikosi kazi kilichopewa jukumu la kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Afrika Mashariki.


-Mtanzania 

DEAR READER LEAVE A COMMENT BELOW

SHARE THIS POSTS TO YOUR FRIENDS BELOW==>>

DONT HESITATE TO JOIN OUR FACEBOOK PAGE BELOW FOR MORE BREAKING AND HOT RESEARCHED NEWS

0 comments em “Tanzania yawalaumu waasi wa M23 kwa kuifanya itengwe jumuiya ya Africa Mashariki”

Post a Comment

 

Mambomseto Copyright © 2011 -- Template created by MAMBOMSETO TEAM -- Powered by MAMBOMSETO

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter