Thursday, November 7, 2013

Jalada la Sheikh Ponda lasimamisha kesi yake Mkoani Morogoro

 
Kesi yenye mashtaka matatu inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini,Sheikh Ponda Issa Ponda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Morogoro ,imeshindwa kusikilizwa baada ya jalada halisi la kesi hiyo kuitishwa kwenda Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kulipitia upya. 
 
Sheikh Ponda alifikishwa mahakamani hapo mapema asubuhi kwa kutumia usafiri wa basi maalumu la magereza na safari hii kesi yake ilikuwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi,Mary Moyo baada ya hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo tangu awali, Richard Kabate kuhamishiwa mkoani Dodoma.
 
Akitoa maelezo ya kesi hiyo,Hakimu Moyo alisema jalada halisi la kesi hiyo liliitishwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Oktoba 15, mwaka huu kwa ajili ya mapitio na kwamba Mahakama Kuu inamamlaka ya kisheria ya kuitisha jalada lolote na kuongeza kuwa kesi hiyo haitaweza kusikilizwa hadi jalada hilo litakaporudi.
 
Hakimu Moyo alisema kwa sasa kesi hiyo itakuwa ikitajwa tu na suala la mshtakiwa kuletwa ama kutoletwa mahakamani liko chini ya magereza kwani dhamana ya mshtakiwa huyo imefungwa,hivyo ataendelea kuwapo magereza hadi Novemba 21,mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.
 
Mapema baada ya kufikishwa mahakamani hapo, Hakimu Moyo alimuuliza Sheikh Ponda kama ana taarifa zozote kuhusu kutokufika kwa mawakili wake watatu mahakamani hapo ambao ni Batholomew Tharimo, Ignas Punge na Juma Nassor hata hivyo, Sheikh Ponda alidai kuwa hana taarifa zozote kuhusu kutofika kwa mawakili wake.
 
Hata hivyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Sunday Hiela ulidai uko tayari kutoa ushahidi ambao ungeanza na askari namba F4949 DC Kingazi wa Kituo Kikuu cha Polisi. Hata hivyo, shahidi huyo hakuweza kutoa ushahidi wake kutokana na jalada halisi la kesi hiyo kutokuwapo mahakamani hapo kwa sababu zilizotolewa awali.
 
Pamoja na kutokufika kwa mawakili wote watatu pia idadi ya wafuasi wa Shekh Ponda ilionekana kuwa ndogo.
 
Sheikh Ponda anakabiliwa na mashtaka ya kutokutii amri halali ya mahakama,kutoa maneno yenye nia ya kuharibu imani za dini na kushawishi watu,makosa hayo kwa pamoja anadaiwa kuyatenda Agosti 10, mwaka huu.

DEAR READER LEAVE A COMMENT BELOW

SHARE THIS POSTS TO YOUR FRIENDS BELOW==>>

DONT HESITATE TO JOIN OUR FACEBOOK PAGE BELOW FOR MORE BREAKING AND HOT RESEARCHED NEWS

0 comments em “Jalada la Sheikh Ponda lasimamisha kesi yake Mkoani Morogoro”

Post a Comment

 

Mambomseto Copyright © 2011 -- Template created by MAMBOMSETO TEAM -- Powered by MAMBOMSETO

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter