HOFU imezidi kutanda kwa wakazi wa Mkoa wa Geita kufuatia matukio ya watu waliofariki dunia na kuzikwa miaka iliyopita kuibuka wakiwa hai.
Mgonda Thomas (22), aliyefariki dunia kwa kujinyonga Mei 28, mwaka jana na kuzikwa siku iliyofuata, Ijumaa iliyopita aliibukia karibu na mlango wa nyumbani kwao akiwa hai.
Tukio hilo ambalo bado la moto, lilijiri katika Kijiji cha Rumasa, Kata ya Buseresere, wilayani Chato mkoani Geita.
Kwa mujibu wa chanzo, majirani ndiyo waliomshuhudia Mgonda akitembea barabarani saa tisa alasiri hatua chache kutoka kwenye mlango wa nyumba hiyo huku nguo zake zikiwa zimechakaa.
Baba mzazi wa kijana huyo, mzee Thomas Msalaba (60) akizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema majirani hao ndiyo waliomtaarifu kwamba mwanaye Mgonda alikuwa barabarani.
“Niliondoka kwenda kumshuhudia kama kweli ni mwanangu. Nilipofika, nilimchunguza kwa umakini sana na kubaini alikuwa yeye.
“Alama kubwa iliyokuwa kwenye mwili wa mwanangu ni kovu kwenye mkono wake wa kushoto lililotokana na kuungua moto, pia sura yake ilifanana sana na mama yake,” alisema mzee huyo.
Naye mama mzazi wa Mgonda, Martha Kitobelo alimthibitishia mwandishi wetu kuwa kijana huyo ni mwanaye kweli.
Familia hiyo ilisema Mgonda alifariki dunia kwa kujinyonga kwa kutumia kamba aliyoifunga juu ya mti wa mwembe hatua chache kutoka nyumbani kwao. Haikujulikana chanzo cha kujinyonga.
Mzee Msalaba alisema kuwa, baada ya Mgonda kufariki dunia alizikwa kwenye makaburi ya nyumbani kwao na siku ya tatu ndugu walianua matanga.
Kufuatia hali ya Mgonda kuwa ya mawengemawenge na kushindwa kuzungumza, wazazi wake walimchukua na kumpeleka kwa mganga wa kienyeji wa eneo hilo aitwaye Juma Tabiho.
Mganga huyo alisema kijana huyo hakufa bali alichukuliwa msukule na maiti waliyoizika ilikuwa kiini macho.
Hata hivyo, katika tukio hilo Jeshi la Polisi Wilaya ya Chato likiongozwa na Mrakibu wa Polisi Wilaya, OCD Leonard Nyaoga lililazimika kufanya kazi ya ziada kuwatuliza wananchi waliopandwa na hasira waliotaka kufukua kaburi ili kuona kilichokuwa ndani.
Afande Nyaoga aliwaambia wananchi hao kwamba kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi na kuwaeleza kuwa chombo chenye uwezo wa kutoa kibali cha kufukua kaburi ni mahakama peke yake.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Pudensiana Protas alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea ikiwa ni pamoja na kufanya utaratibu wa kumpima DNA kijana huyo ili kujiridhisha kama kweli ndiye Mgonda aliyefariki dunia mwaka jana.
Hili ni tukio la tatu kutokea mkoani Geita katika kipindi kisichozidi miaka mitano iliyopita.
Aprili 12, 2013 katika Kijiji cha Kasamwa wilayani Geita, Flora Onesmo (45) aliyefariki dunia Februari 28, 2008 aliibuka akiwa hai.
Septemba 28, mwaka huu aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Mwatulole mjini Geita, Shaban Maulid (16) aliyefariki dunia Januari 1, 2011 naye aliibukia Mtaa wa Mbugani jirani na nyumbani kwao, Kata ya 14, Kambarage mjini Geita.
Kufuatia matukio hayo yenye dalili za ushirikina, Askofu wa Kanisa la Zion Assemblies of God Geita, Edward Osako alisema katika maandiko hakuna binadamu aliyewahi kufa kisha akafufuka zaidi ya Lazaro aliyefufuliwa na Yesu akiwa kaburini.
“Haya matukio ya watu kufa na kuonekana wakiwa hai baada ya miaka kadhaa ni nguvu za giza ambapo hata kwenye Biblia yameandikwa,” alisema Askofu Osako.
-GPL
DEAR READER LEAVE A COMMENT BELOW
SHARE THIS POSTS TO YOUR FRIENDS BELOW==>>
DONT HESITATE TO JOIN OUR FACEBOOK PAGE BELOW FOR MORE BREAKING AND HOT RESEARCHED NEWS