Kama ni kweli hii ni habari njema! Siku chache baada ya kuliambia gazeti ndugu la hili, Amani kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa chango hivyo inambidi azae, super lady wa sinema za Kibongo, Ruth Suka ‘Mainda’ anadaiwa kuwa mjamzito, Ijumaa Wikienda limechimba kila ‘engo’.
Super lady wa sinema za Kibongo, Ruth Suka ‘Mainda’.
MUONEKANO
Habari zilieleza kwamba kimuonekano, Mainda aliyezoeleka kuonekana mwembamba, sasa ameanza kunenepa huku kitumbo nacho kikianza kuwa kikubwa.
Habari kutoka kwa mmoja wa mashosti zake aliyeomba hifadhi ya jina, zilidai kwamba kila amuonapo Mainda anagundua kuwa ana mabadiliko fulani ndani ya mwili wake hasa tumbo lake kuongezeka ukubwa.
“Unajua Mainda ni msiri sana hasa katika kipengele cha kuzungumzia mwili wake, kila tukimuuliza shosti wetu kama ni mjamzito anakataa.
“Anadai eti ana matatizo ya ugonjwa wa chango lakini ukimwangalia tumbo unaona linazidi kukua, binafsi mimi naamini ni mjamzito ila yeye anafanya siri,” alidai rafiki huyo.
APELEKWA HOSPITALI
Habari zilizoenea Ijumaa iliyopita zilidai kuwa mwanadada huyo alipelekwa kwenye Hospitali ya Kinondoni maarufu kwa jina la kwa Dokta Mvungi jijini Dar.
Siku hiyohiyo mwanahabari wetu alizama hospitalini hapo ambapo alikutana na vizuizi vingi kwa kuwa moja ya masharti huruhusiwi kuingia wodini bila kufuatana na ndugu wa mgonjwa.
Katika jitihada za kuthibitisha kama Mainda kalazwa hapo na kujua kinachomsumbua, mmoja wa madaktari (jina linahifadhiwa) ambaye anamfahamu mwandishi wetu alimtonya kuwa ni kweli Mainda alifikishwa hospitalini hapo.
UGONJWA, UJAUZITO
Kuhusu ugonjwa uliompeleka hospitalini hapo na habari kuwa ni mjamzito, dokta huyo alisema: “Ninavyojua mimi, ugonjwa ni siri ya daktari na mgonjwa au na ndugu. Nadhani muulize mwenyewe, akipenda atakwambia. Ni kweli alikuwepo na amesharuhusiwa.”
Ijumaa Wikienda lilimtafuta Mainda kwa njia ya simu lakini akawa hapokei.
Baadaye mwandishi wetu alikwenda hadi nyumbani kwa Mainda, Kijitonyama, Dar lakini alijibiwa na majirani kuwa hayupo kwa muda mrefu.
APOKEA SIMU
Hata hivyo, juhudi za kumpata, ziliendelea ambapo alitumiwa ujumbe mfupi, alipopigiwa akapokea.
Katika mazungumzo yake na mwandishi, Mainda alikiri kuwa anasumbuliwa na chango na kwenda hospitali lakini alikataa kuzungumzia ishu ya ujauzito.
“Mimi nilishasema nasumbuliwa na chango, huo ujauzito unaosema, hata kama upo, tusubiri kwani huwa haufichiki,” alisema Mainda.
UTATA
Baada ya habari kuwa ya mjini, ishu hiyo iliibua utata kuwa kama ni ugonjwa wa chango, inawezekana mtu akazidiwa kiasi hicho hadi kukimbiza hospitali?
Pia ilihojiwa kuwa kama kweli ni mjamzito, je, baba wa kiumbe hicho ni nani?
NI MIMBA YA PILI?
Kama kweli Mainda atakuwa mjamzito basi itakuwa ni mimba ya pili baada ya kukiri kuwa aliwahi kuchoropoa ya aliyekuwa mtu wake, mwigizaji Vincent Kigosi ‘Ray’ ambaye walishamwagana.
GPL